Friday, May 11, 2007

Urasimu katika utoaji habari uachwe

Tahariri

MhaririHabariLeo; Thursday,May 03, 2007 @00:01
LEO ni Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, siku ambayo waandishi na watu wote duniani wanaungana kukumbushana umuhimu wa habari katika maendeleo ya nchi yoyote katika dunia hii na haja ya kuhakikisha uhuru katika utoaji na kupokea habari haupokonywi na mtu yeyote.

Wakati kwa mwaka huu tathmini inayofanyika ni matatizo ya usalama yanayowakabili waandishi, wahariri na wachapishaji wanaojitolea maisha yao katika kuhakikisha wanawapatia wananchi taarifa muhimu, na kadhalika inasikitisha kwamba waandishi wameendelea kupoteza maisha yao kwa wingi katika utendaji wa kazi zao. Kwa mfano, ripoti ya mwaka jana inaonyesha kuwa waandishi wa habari 150 waliuawa mwaka jana na mamia wengine walikamatwa, kutishiwa na kushambuliwa kutokana na ukiukwaji wa uhuru wa vyombo vya habari katika sehemu mbalimbali duniani.

Kama tulivyosema hiyo ni hali ya kusikitisha, lakini ambayo haiwezi kuachwa ivuruge jitihada za utoaji habari kwa jamii. Ukiachilia mbali sura ya dunia katika suala zima la habari, hapa kwetu Tanzania hali nayo haijawa barabara.

Tunasema haijawa barabara kwa kuzingatia kwamba maofisa wa serikali bado wanaendelea na urasimu wao wa kutoa habari. Wanaendelea kuwa wagumu wa kutoa habari licha ya Rais Jakaya Kikwete kuwaeleza – zaidi ya mwaka mmoja uliopita – kwamba wanapaswa kuwa na mfumo unaohakikisha wanatoa habari kwa waandishi inavyotakiwa.

Kwa mfano katika wizara na idara za serikali maelekezo yalikuwa ni kwamba wawe na vitengo kama siyo maofisa wanaohusiana na habari kurahisisha mawasiliano na waandishi na vyombo vya habari. Lakini bahati mbaya ni kwamba hata katika wizara ambazo kuna vitengo au maofisa wa aina hiyo bado urasimu katika utoaji habari uko vile vile.

Limekuwa ni jambo la kawaida kwa maofisa wa aina hiyo kuwataka waandishi kuandika maswali hata wanapotaka kupata ufafanuzi wa suala la kawaida tu! Hivyo tunasema katika kuadhimisha siku ya leo, ingefaa wizara na idara za serikali zibadilike na kwenda na wakati. Waache urasimu katika utoaji habari ili kuleta maendeleo halisi ya wananchi na taifa kwa ujumla.

No comments: